Watu wawili,Godson Josea -Msimamizi wa mradi wa maji wa Shimbi Mashariki na Mhandisi Amos Thomas walio chini ya Mkandarasi HECO SANMARK (T) LTD wanashikiliwa na jeshi la polisi mpaka Mkandarasi huyo atakapojisalimisha kwenye uongozi wa wilaya.
Maamuzi hayo yamefanywa na Naibu waziri wa Maji Jumaa Aweso baada ya kufika katika mradi wa maji Shimbi Mashariki na kukuta mradi ulioanza toka mwaka 2013 haujakamilika na mkandarasi ambaye amekwishalipwa fedha na serikali kiasi cha shilingi milioni 100 hayupo eneo la mradi, huku kukiwa na malalamiko ya vibarua kutokulipwa fedha zao.
Aidha Naibu Waziri Aweso amemuagiza Mhandisi wa RUWASA Joseph Mcharo kuhakikisha anafuata taratibu za kisheria na kuvunja mkataba na HECO SANMARK (T) LTD pindi atakapojisalimisha ili asilimia 12 zilizobaki za mradi kukamilika zifanywe na wataalamu wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi Wa Mazingira (RUWASA)Wilaya ya Rombo .
Ameongeza kuwa mbali na kushughulikia suala la vibarua kulipwa fedha zao , pia RUWASA wanatakiwa kuhakikisha mzabuni wa pampu za maji analipwa fedha yake na pampu ziwashwe ili wananchi wa eneo hilo wapate huduma maji.
Mhandisi Mcharo amesema kuwa mradi wa maji Shimbi Mashariki wenye thamani ya shilingi milioni 887.4 umeshatekelezwa kwa asilimia 88 huku Mkandarasi akiwa amekwishalipwa kiasi cha zaidi ya milioni 400 na anadai kiasi cha shilingi milioni 86 tu.
Amesema sababu kubwa wanayoitoa wakandarasi ya kuchelewa kukamilisha miradi ni kutolipwa madai yao kwa wakati , na pindi wanapoandikia madai yao wanasimamisha ujenzi mpaka walipwe fedha zao ndio waendelee na kazi.
Vilevile Naibu Waziri Aweso alitembelea mradi wa maji katika kijiji cha Leto wenye thamani ya shilingi milioni 927.9 ambao nao pia haujakamilika kitu kinachosababisha wanakijiji wa eneo hilo kwenda kuchota maji nchi jirani ya Kenya.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved