Uzinduzi wa kampeni ya Pima, Jitambue, Ishi Wilaya ya Rombo ulifanyika siku ya tarehe 25.09.2018 katika viwanja vya stendi ya mabasi Mkuu ikiwa ni kampeni ya Kitaifa yenye lengo la kufikia asilimia 90 ya watanzania ambao wamepimwa VVU na kujua hali zao ifikapo mwaka 2020 na kundi la kwanza linalolengwa ni wanaume, likifuatiwa na vijana wa kike kuanzia miaka 15 hadi 25 na kundi la tatu ni wanawake wajawazito.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mhe. Agnes Hokororo amewaomba wanaume wa Rombo kujitokeza kwa wingi na kupima hali zao na kuacha kuwategea wake zao kwasababu ni muhimu katika familia au kaya zetu kuhakikisha kila mmoja wetu ametambua afya yake .
“Takwimu za kitaifa zinaonesha wanaume wamekuwa na muitikio mdogo wa kupima VVU na kuwaachia wanawake hasa wakinamama wajawazito jukumu la kupima afya zao na wanapokutwa hawana maambukizi na wao wanajihakikishia kuwa wako salama kupitia vipimo vya wake zao.” Alisema Hokororo
Aliongeza kuwa kuna faida kubwa ya kujua hali ya afya zetu na iwapo ukikutwa na maambukizi kuanza dawa mapema ni mwili kuweza kupambana na virusi vinavyosababisha UKIMWI na kufubaa mapema hatimaye kupunguza kiwango cha virusi mwilini.
“Ninachukua fursa hii kuishukuru serikali chini ya Wizara ya Afya, Jinsia , Wazee na Watoto kwa kubuni na kufanya kampeni hii lakini pia nichukue fursa hii kuwaomba sana viongozi wa dini mbalimbali kusaidia kushawishi waumini wao kupima afya ili kufahamu hali zao”, alimalizia Hokororo
Naye Mratibu wa UKIMWI Wilaya ya Rombo Dkt Agripina Masao alisema kuwa zoezi la upimaji la kitaifa lenye kauli mbiu ya “Furaha yangu; Pima, Jitambue, Ishi” litaendelea mpaka novemba 30 mwaka huu ambapo kiwilaya tumepewa malengo ya kuhakikisha tumepima watu 6,689.
Ameongeza kuwa zoezi hili lilianza toka tarehe 17 Septemba na mpaka tarehe 23 Septemba watu 236 walijitokeza kupima na hakuna na aliyekutwa na maambukizi na zoezi litaendelea kufanyika mpaka Novemba 30 , 2018 kwenye Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali zote zinazotoa huduma ya kupima VVU.
Lengo kuu la kampeni hii ya kitaifa ni kutekeleza mikakati ya kufikia 90 tatu yaani 909090 ifikapo mwaka 2020, 90 ya kwanza ikiwakilisha asilimia ya watu watakaojitokeza kupima VVU na kujua hali zao za maambukizi, 90 ya pili ni asilimia ya watu waliokutwa na maambukizi na kuanza dawa mara moja, 90 ya tatu ni asilimia ya watu wanaotumia dawa kwa uaminifu ili waweze kuwa na kiwango kidogo cha Virusi Vya UKIMWI.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved