Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo limeazimia kuvunja mkataba baina ya Halmashauri na Kampuni ya maji ya Kiliwater inayosimamia na kuendesha miradi ya maji Rombo kwa kushindwa kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Rombo.
Sambamba na hilo baraza limetoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji kuunda kamati maalumu itakayokwenda kuonana na Waziri wa maji ili kuunda mamlaka ya maji Rombo itakayokua inapata ruzuku serikalini ili kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi.
Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya baadhi ya madiwani kuwasilisha hoja maalum katika baraza la madiwani lililofanyika mnamo tarehe 05.02.2019 katika ukumbi wa Halmashauri na Baraza la Madiwani kujadili hoja hiyo kwa kina.
Aidha Mhandisi wa Maji (W) John Msengi amelieleza baraza la madiwani kuwa Kampuni ya Kiliwater ipo kwa ridhaa ya warombo wenyewe baada ya serikali kujiondoa katika majukumu ya uendeshaji wa miradi ya maji moja kwa moja na kuwataka wananchi wenyewe waamue na wakaamua kuipa dhamana hiyo kampuni ya Kiliwater.
Akifafanua hilo amelieleza baraza la madiwani kuwa kabla ya mabadiliko ya sera mwaka 1995 serikali ilikuwa na majukumu makuu matatu ambayo ni sera na mipango, pili ni ujenzi wa miradi ya maji, upanuzi na ukarabati mkubwa na tatu ni uendeshaji na usimamizi ambapo baada ya mabadiliko ya sera Wizara iliona serikali inapata gharama kubwa kuendesha moja kwa moja na kuanzisha sera ya kuundwa vyombo huru vitakavyosaidia kusimamia na kuendesha miradi ya maji kama vile mamlaka , watu binafsi na makampuni .
Baada ya mchakato wa kuunda vyombo hivyo kukamilika serikali ilihamisha jukumu la tatu la uendeshaji na usimamizi kwa kampuni pamoja na kuwapa vitendea kazi, na serikali kuendelea kuisimamia Kampuni kwa utaratibu na makubaliano waliyoyaweka katika andiko .
Hata hivyo Mhe Gaston Mtuta Diwani wa Kata ya Reha ambae ndiye aliyewasilisha hoja hiyo alisema kuwa kampuni ya Kiliwater haijawahi kukaguliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), haina wafanyakazi wenye ujuzi wa kutosha na haiwajibiki kwa wananchi.
Ameongeza kuwa kampuni inazalisha maji lita za ujazo 18,000 kwa siku kipindi cha kiangazi na lita 22,000 kipindi cha masika wakati hali halisi ya mahitaji ya huduma hiyo kwa wananchi ni lita za ujazo 40,000 kwa siku hii inaonesha wazi kampuni haiwezi kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Rombo.
Naye Meneja wa Kiliwater (W) Prosper Kessy ameikanusha madai ya kampuni kutowajibika kwa wananchi ambapo amesema kuwa vikao vinafanyika kila mwaka na kamati za maji katika kila kijiji katika tarafa husomewa taarifa mbalimbali za utekelezaji, mipango ya kampuni pamoja na changamoto ,vyote vinawekwa wazi na wananchi wanashiriki kikamilifu.
Aidha amelihakikishia Baraza la Madiwani kuwa Kampuni ya Kiliwater ina wataalamu wa kutosha wenye elimu kubwa na wanafanya kazi kwa weledi mkubwa. Na taarifa zote za utekelezaji wa majukumu huwasilishwa kuanzia ngazi ya Halmashauri,mkoa mpaka Wizara.
Kessy amesisitiza kuwa kampuni ipo kutoa huduma na sio kibiashara na kama utaratibu wa Makampuni ulivyo ni budi kukaguliwa na wakaguzi huru wa hesabu za Fedha na kutolewa taarifa , na hilo limekuwa likifanyika kwa Kampuni ya Kiliwater toka ilipoanzishwa.
Pamoja na hayo Kessy amesema ili kampuni ifanye vizuri inatakiwa kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wote wa maji ikiwa ni pamoja na kuwa walinzi wa miundombinu ya maji na wao kama Kampuni watajitahidi kuboresha huduma ya maji kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved