Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Dr.Jim Yonazi pamoja na timu yake imefanya ziara wilayani Rombo ili kukagua tatizo la mwingiliano wa mawasiliano ya simu na redio yaliyopo katika wilaya na kuangalia maeneo yanayohitaji huduma ya mawasiliano na maeneo yanayohitaji maboresho.
Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 30 Machi mwaka huu Dr Yonazi amesema kuwa serikali inafanyia kazi tatizo la mwingiliano wa mawasiliano na muda si mrefu maeneo yote yatakuwa na usikivu mzuri wa mawasiliano ya simu, redio na Televisheni.
Mawasiliano ni uchumi,na yanapokuwa mazuri wananchi watashiriki vema katika shughuli za kiuchumi na kuleta maendeleo, hivyo serikali kwa kushirikiana na makampuni ya simu inaendelea kujenga minara na kuboresha mawasiliano hasa katika maeneo ya mipakani ambapo ndio kuna mwingiliano mkubwa wa mawasiliano, alisema Dr. Yonazi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Peter Ulanga alieandamana na Dr. yonazi katika ziara hiyo amesema kuwa, wao kama mfuko wana jukumu la kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hayana mvuto kibiashara.
Ameongeza kuwa , kazi kubwa iliyopo ni kuyatambua maeneo hayo na kutenga ruzuku kwa kushirikiana na makampuni ya simu ili kuongeza usikivu wa mawasiliano,kuongeza shughuli za kibiashara maeneo ya mpakani na kuimarisha ulinzi ambapo katika wilaya ya Rombo tayari mradi umefanyika na katika miezi michache ijayo miradi mingine ya kuongeza usikivu katika wilaya itafanyika.
Hata hivyo amesema kuwa eneo kubwa la Rombo lina mlima Kilimanjaro ambao umekuwa kama ukuta na kuzuia mawasiliano kutoka sehemu nyingine, lakini tayari kwa upande wa redio kuna ushirikiano na TBC kuhakikisha redio za Tanzania zinasikika katika maeneo mbalimbali hivyo wataangalia jinsi ya kuongeza vituo zaidi vya mawasiliano katika wilaya ya Rombo.
Nao viongozi mbalimbali katika wilaya ya Rombo akiwemo katibu tawala wilaya ndugu Abubakar Assenga pamoja na Diwani wa kata ya Motamburu Kitendeni Mhe. Abdallah Mbago walikiri kuwa mwingiliano wa mawasiliano katika wilaya ya Rombo upo kwa kiwango kikubwa na baadhi ya maeneo inasoma mitandao ya Kenya na hata redio wanasikiliza za Kenya.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved