Katika harakati za kupambana na athari za utapiamlo na kuboresha hali ya lishe katika wilaya ya Rombo, kamati ya lishe wilaya chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, imejipanga kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wote kuhakikisha athari za utapiamlo zinapungua.
Akizungumza mara baada ya kufungua kikao cha kamati ya lishe wilaya, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Ndugu Chrispin Mng’anya amesema kuwa ni vyema elimu ya lishe itolewe kwa wamama wanaonyonyesha na wajawazito ili watoto wanapozaliwa wawe tayari mama zao wanaelewa umuhimu wa lishe bora kwa watoto.
“Siku elfu moja(1000) za mwanzo za maisha ya mtoto ni msingi wa lishe bora kwa mtoto na lishe isipozingatiwa katika muda huo inaathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili”, alisema Mng’anya.
Aliongeza kuwa agenda ya lishe iwe ya kudumu kwenye vikao vinavyofanyika katika maeneo yetu ikiwa ni pamoja na uwepo wa timu maalum katika kila ngazi itakayosaidiana na Afisa Lishe kutoa elimu ya lishe kwa jamii.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya, Bw. Boaz Mwaikugile amesema kuwa kutokuwa na mpangilio mzuri wa chakula na lishe kwa ujumla kunaweza kusababisha maradhi mengi katika mwili wa binadamu likiwepo tatizo la utapiamlo.
“Magonjwa mengi yanayowapata binadamu yana uhusiano mkubwa sana na suala la lishe, mbali na tatizo la utapiamlo kuna maradhi kama vile kisukari, shinikizo la damu na mengine mengi”alisema Mwaikugile
Naye Mhandisi wa maji(W) Bw John Msengi ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo ameshauri kabla ya kamati kuanza kazi rasmi ya kupambana na utapiamlo ni vema kufanya uchunguzi na kutambua ukubwa wa tatizo la utapiamlo kiwilaya na takwimu zioneshe maeneo yenye shida zaidi ili nguvu kubwa ielekezwe katika maeneo hayo.
Hali ya utapiamlo inasababishwa na ukosefu wa lishe/chakula bora pamoja na maambukizi ya mara kwa mara yanayosababisha mtu kukosa hamu ya kula na kushindwa kula mlo kamili. Wakina mama wajawazito na wanaonyonyesha wapo kwenye hatari zaidi ya ya kupata utapiamlo na watoto wadogo wanaweza kuathirika toka tumboni iwapo mama hakupata lishe bora kabla na wakati wa ujauzito.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved