Mkuu wa wilaya ya Rombo Mhe Agnes Hokororo ametangaza mapambano endelevu dhidi ya uzalishaji wa pombe haramu ya gongo pamoja na pombe za ndizi zisizo na viwango alipokuwa akiongoza kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya( DCC) kilichofanyika tarehe 5 octoba mwaka huu .
Akizungumza katika kikao hicho Mhe.Hokororo amevitaka vyombo vya dola kufanya wajibu wao ikiwa ni pamoja na kukagua ikibidi kuzuia uingizwaji wa malighafi zinazotengeneza pombe hizo kwa mfano molasses ambazo huwa zinaingizwa Rombo kwa kisingizio kuwa ni chakula cha ng’ombe ilihali matumizi halisi ni kutengenezea gongo.
"Sisi sote kama wananchi wenye nia njema na wilaya ya Rombo, basi tushirikiane kwa pamoja kutoa taarifa, kuwakamata ,kuwachukulia hatua na kuwafikisha mahakamani wazalishaji na watengenezaji wa pombe haramu zisizo na TBS", alisema Hokororo
Naye mjumbe mualikwa Bi Faith Sway kutoka WOCHIVI (Women and Child Vision) Taasisi isiyo ya kiserikali inayosaidia kupambana na ulevi uliokithiri, ameshukuru ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwa mkuu wa wilaya pamoja na Afisa Tarafa ya Tarakea ambapo vijiji vya Mbomai na Kikelelwa vinafanyiwa kazi na taasisi hiyo.
Akitoa mchango wa mawazo katika kikao hicho Bi Faith amesema kuwa ulevi uliokithiri unasababisha matatizo mengi katika jamii ikiwemo ubakaji pamoja na ongezeko la maambukizi ya VVU.
Sambamba na hilo Afisa Tarafa Tarakea Ndg Saburi Uledi aliwasilisha taarifa ya msako uliofanyika mwezi Agosti na Septemba, 2018 na kufanikiwa kukamata mitambo 11 ya kutengenezea gongo pamoja na lita 80 za gongo na kesi tatu tayari zipo mahakamani
Wilaya ya Rombo imeendelea kudhibiti uanzishwaji wa kampuni na viwanda bubu vinavyozalisha pombe huku ikifanikiwa kuvifungia viwanda na kampuni katika vijiji vya Shimbi,Lessoroma,Marangu Katangara na Kirongo Chini.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved