Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa hali ya mpaka baina ya Kenya na Tanzania si salama kwa sababu wananchi wengi wanapenda kutumia njia za panya kuingia na kutoka upande mmoja wa nchi kwenda mwingine.
Katika ziara yake wilayani Rombo mnamo tarehe 23.2.2019 Mhe. Majaliwa amewaasa wananchi wa nchi zote mbili kuwa walinzi wa mpaka huo kwa kuhakikisha wanafuata taratibu pindi wanapotaka kuingia upande wa pili na kuacha kutumia njia za vichochoro ambavyo vinafanya mambo ya hovyo na kuhatarisha usalama wa nchi hizi mbili.
“Hali ya ulinzi na usalama katika mpaka huu wa Holili si nzuri na polisi pekee au Jeshi pekee haliwezi kuulinda mpaka huu kwa urefu wote, hivyo ni muhimu sana wananchi kwa ujumla wake wa pande zote mbili kuwa walinzi wa mpaka huu kwa kuhakikisha mnapita katika vituo rasmi vilivyowekwa ili kutoa taarifa za kutoka na kuingia”, Mhe.Majaliwa ameyasema hayo akihutubia wananchi katika eneo la Kastamu Holili.
Ameongeza kuwa, Serikali imeona viashiria mbalimbali vinavyoonesha maeneo ya mpakani hayapo salama, kutokana na matukio ya kutisha yanayotokea katika maeneo ya mipakani nchini, kwa mfano mauaji ya watoto katika mkoa wa Njombe na utekaji wa watoto na kudai fedha katika wilaya ya Kibondo inayopakana na nchi ya Burundi.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya mipaka , na wanaotumia njia za vichochoroni (njia za panya) kupitisha bidhaa ndio wanaoweka na vitu visivyo halali kama mabomu na bunduki, hivyo yeyote atakayekamatwa anapita njia hizo na mafurushi hata kama ni bidhaa za biashara bila kufuata utaratibu atakamatwa na atashughulikiwa.
Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi wa umma hasa maafisa uhamiaji kutojihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo vinasababisha kuruhusu mambo mengi bila kufuata utaratibu kwa sababu nchi zote mbili zipo makini sana katika suala hilo hivyo watumishi wa umma wajiimarishe na iwapo ikibainika serikali haitaunda tume itashughulika na muhusika papo hapo.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved