Mkuu wa wilaya ya Rombo Mhe. Agnes Hokororo amepiga marufuku kwa wananchi kuruhusu mifugo kutoka nchi jirani ya Kenya kufanya malisho mashambani na kufanya uharibifu wa mazao ya chakula ,kwa sababu wakaazi wa Rombo wanafanya ufugaji wa ndani hivyo si vema kuruhusu mifugo ya watu wengine kuzurura.
Ameyasema hayo alipokuwa anasikiliza kero mbalimbali katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Kiwanda mapema leo ,ambapo wananchi walilalamika mazao yao kuliwa yakiwa shambani na mifugo kutoka nchi jirani ya Kenya ,na wanapokuja kulisha mifugo wanakuja na silaha mbalimbali kama mapanga na sime.
Ameongeza kuwa pale inapotokea kuna makubaliano ya kibiashara ya kuuziana malisho kati ya Mkenya na Mtanzania basi ni vema aandaliwe kwa kukatiwa majani au mahindi na kupewa aondoke nayo ili kuepusha uharibifu wa mazao ya wengine mashambani kwa kuwa anapoingiza mifugo shambani hawafanyi malisho eneo moja tu walilouziwa bali wanaharibu na mazao ya mashamba jirani.
“Uharibifu wa chakula ni uharibifu wa mali kama zilivyo mali zingine, Kaimu Kamanda wa Polisi wilaya nakuagiza, kama ambavyo tunakamata wahalifu katika maeneo mengine na hawa ni wahalifu vilevile kwasababu chakula ni hitaji muhimu katika jamii kwa maendeleo ya kila siku”.alisema Hokororo
Pamoja na hilo ameushauri uongozi wa kijiji kuunda kamati imara ya kusimamia masuala ya mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi wa kutosha kwa kila mtu kuwa mlinzi wa jirani yake ili kuwatambua wanaoruhusu malisho kwenye mashamba bila idhini ya wenye mashamba.
Wizara ilishatoa onyo kuhusu mifugo kuzurura ovyo pamoja na maelekezo ya kufuata sheria za NARCO ambazo zinaelekeza gharama za kuchangia mifugo inapofanya uharibifu wa mazingira, nyasi walizokula , maji na mengineyo.
Kwa upande wa wanyama waharibifu kama Nyani, Mhe. Hokororo amemuagiza Afisa Ardhi,maliasili na mazingira kutafuta mbinu mbadala ya kuwafukuza bila kuwadhuru ili wasiendelee kuharibu mazao,
Vile vile amewaelekeza wananchi pindi wanyama wakubwa kama Tembo na wengine wanapokuja kushambulia basi ni budi kuandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ili wizara husika ipewe taarifa kwa ajili ya fidia inayotolewa kwa mujibu wa sheria
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved