Jani la sale ni maarufu miongoni mwa kabila la wachaga, ni jani linaloheshimika sana katika kutatua migogoro na kuombea msamaha . Kwa imani za kichaga mtu yeyote aliyekosea akienda kuomba msamaha na jani la sale basi ni budi asamehewe. Lakini pia jani hili hutumika kuwekea mipaka ya maeneo na kukaribishia wageni kama viongozi wa dini na serikali kuashiria amani .
Jani hili ambalo kwa uhalisia wake lilikua linasaidia kudumisha amani, upendo na mshikamano miongoni mwa kabila la wachaga limegeuka kuwa shubiri katika jamii ya wachaga kwasababu limekuwa likizorotesha mchakato mzima wa kutafuta haki, na linachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matendo ya ukatili pamoja na mimba za utotoni.
Kamati ya MTAKUWWA( Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto) wilaya ya Rombo imeazimia kuundwa kwa sheria ndogo dhidi ya matumizi ya Jani la sale kwenye kesi za ukatili wa kijinsia, baada ya kuonekana kesi nyingi za ulawiti, ubakaji na mimba zinamalizwa kimila kwa kutumia majani hayo.
Aidha baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wamesema kuwa jani la sale limekuwa halitumiki tena kama jani la amani bali ni kama jani la kuvunia fedha,kwani katika mchakato wa kutatua kesi kimila sio jani la sale pekee linalotumika huwa linaambatana na fedha au mifugo ili mhusika kusamehewa.
Pamoja na hilo kuna baadhi ya wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA walilishutumu jeshi la polisi wilaya ya Rombo kwa kuzorotesha upatikanaji wa haki kwa kutoshirikiana na wananchi kupinga vitendo vya ukatili kwa kuwaachia huru watuhumiwa.
Katika kujibu tuhuma hizo Mkuu wa Polisi (W) Ndg Ally Kitole ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, amesema kuwa hakuna kitu kinachomshangaza kama kesi za Jinai kutatuliwa kimila hasa kwa kutumia majani ya Sale, na kuongeza kuwa haki jinai haitegemei mtu mmoja kupatikana, na wananchi ndio wamekuwa wakichangia kukwamisha mchakato mzima wa kupata haki , kwani muathirika mwenyewe ndio anakuwa wa kwanza kutotoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Rombo Mhe. Agness Hokororo akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya kilichofanyika Nov,15 2019 ameelezea masikitiko yake juu ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili na ukwamishaji wa haki pale ambapo wananchi wanakwamisha mchakato wa utafutaji wa haki kisheria.
Amesema kuwa kesi nyingi za ulawiti na ubakaji katika mahakama ya wilaya zimeshindwa kuendelea kutokana na mzazi (mama) anapoitwa mahakamani kutoa ushahidi, wamekuwa wanaficha ukweli,hivyo kufifisha haki za watoto wao hasa pale wanapoamua kukubaliana na kumalizana na watuhumiwa.
Aidha Hokororo amezungumzia vitendo vya ukatili na mauaji ambavyo vimekithiri katika wilaya ya Rombo hasa katika Tarafa ya Usseri ambapo kwa mwaka huu 2019 kuanzia Aprili hadi July jumla ya watu wasiopungua nane (8) waliuawa na kwa bahati mbaya jeshi la polisi lilishindwa kuhakikisha wahusika wanatiwa nguvuni kwa sababu walikosa ushirikiano kutoka kwa wananchi.
Sambamba na hilo ameongelea matukio ya wanaume kujinyonga katika eneo la Rombo , kitu ambacho pengine kwa kiasi kikubwa kinachangiwa na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wanavyofanyiwa wanaume, huku akisisitiza kuwa matendo ya ukatili na unyanyasaji wanafanyiwa makundi yote hata wababa lakini hayaripotiwi.
Hokororo ametoa rai kwa viongozi wa dini wasisite kusemea wazi wazi vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika makanisa na misikiti kwa kutumia maandiko ya dini ili jamii ibadilike, kwa sababu matendo hayo ni kinyume na mpango wa Mungu.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved