Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amefanya ziara wilayani Rombo na kukagua usikivu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC) , ikiwa ni pamoja na kutembelea mtambo wa kurushia matangazo uliopo katika eneo la Tarakea.
Dkt .Mwakyembe amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 E imeweka wazi jukumu la serikali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa. Na kwa kutambua hilo wizara kwa kushirikiana na sekta ya mawasiliano iliunda timu iliyopita kukagua maeneo yote ya mipakani ambayo ndio yenye shida ya kupata usikivu na kukuta wanasikiliza redio za nchi jirani.
Baada ya kupita timu hiyo Dkt Mwakyembe amesema kuwa changamoto za usikivu zilitatuliwa katika maeneo mengi lakini bado serikali iliendelea kupata malalamiko katika maeneo ya Rombo na Loliondo na baada ya timu ya pili kupita pia iligundua bado maeneo hayo hayana usikivu.
‘Kwa wilaya ya Rombo ni lazima kufanya uwekezaji zaidi, kwa kuweka Mtambo zaidi ya mmoja na kuuongezea nguvu Mtambo wa kurushia matangazo uliopo Moshi ili eneo lote la Rombo lipate usikivu wa TBC’, amesema Dkt. Mwakyembe.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBC, Mhandisi wa Ufundi Upendo Mbelle amekiri kuwepo kwa changamoto ya usikivu katika baadhi ya maeneo baada ya Shirika kufanya ukaguzi wa mitambo na kubaini changamoto ya kila mtambo.
Ameongeza kuwa TBC imejipanga kufanya maboresho katika mitambo yao na tayari vifaa vyote vinavyotakiwa vimeshanunuliwa, kwa sasa vinafanyiwa uhakiki na ndani ya miezi mitatu kazi ya maboresho itakuwa imekamilika.
Aidha kwa upande wa wilaya ya Rombo Mhandisi Mbelle amesema kuwa maboresho yatafanyika katika mtambo wa kurushia matangazo uliopo Moshi ili usikivu ufike mpaka eneo la Holili, na vilevile wataongeza mtambo mwingine katika eneo la Mkuu ili eneo lote la Rombo lipate usikivu.
Awali akimkaribisha Dkt Mwakyembe , Mkuu wa wilaya ya Rombo Agness Hokororo amesema kuwa kero kubwa kwa wananchi wa Rombo baada ya Maji ni mawasiliano, kitu kinachoweza kupelekea watu kupashana habari zisizo sahihi.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved