Meya wa Manispaa ya Alvsbyn (katikati) Bi Helena Ohlund na Mhe.Diwani Severine Lasway wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo (Kulia) wakitia saini makubaliano ya ushirikiano huo kushoto ni Mh.Diwani Simon Kinabo wa Rombo
Halmashauri ya wilaya ya Rombo na Manispaa ya Älvsbyn ya nchini Sweden imesaini makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano katika vipengele vitano ambavyo ni ukuaji wa miji na mipango miji, mazingira,huduma za afya kwa vijana, utalii wa asili na usalama wa chakula. Ambapo vipengele vitatu vya mazingira,usalama wa chakula na huduma za afya kwa vijana vitaanza kufanyiwa utekelezaji kuanzia mwezi wa tisa 2018.
Ushirikiano huu mpya ulioanzishwa kati ya Älvsbyn na Rombo unafadhiliwa na ICLD, Kituo cha Kimataifa cha Demokrasia ya Mitaa. Mpango huu ni kuwezesha ushirikiano kwa angalau miaka mitano, anaelezea Linda Öhlin, meneja wa mradi.
Wawakilishi wanne kutoka wilaya ya Rombo walialikwa kufanya ziara fupi katika manispaa ya Alvsbyn mwezi mei mwaka huu. Wawakilishi hao ni Mkuu wa wilaya Bi Agness Hokororo ambaye pia alikuwa Mkuu wa msafara, Mh.Diwani Severine Lasway (Mwenyekiti, kamati ya Elimu ,Afya na Maji), Mh.Diwani Simon Kinabo (Mwenyekiti, kamati ya Uchumi, ujenzi na mazingira) pamoja na Mathias Gungumka ambaye ni Afisa Usafi na Mazingira wa wilaya.
Katika ziara hiyo timu ya Rombo ilijifunza mambo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira kwa kuchakatisha taka kuwa malighafi za viwandani ambapo mbali na kutunza mazingira pia ni njia ya kuongeza kipato.
Vile vile walijifunza jinsi ya kuongeza thamani bidhaa za chakula na bidhaa nyingine kwa ubora wa viwango vya juu pamoja na upatikanaji na usambazaji wa maji salama na safi kwa kutumia teknolojia ya tarakinishi (computer) ili kupunguza gharama za uendeshaji wa sekta hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo Bi. Agness Hokororo alisema kuwa ziara ya Alvsbyn ilikuwa ya kuvutia na yenye kuongeza ujuzi na inaonekana kuwa ni sehemu yenye watu wanyenyekevu na wachapakazi ndio maana hawakuweza kuona watu wengi muda wa mchana hali ambayo ni nzuri.
"Nimevutiwa na nidhamu ya waswideni ya kuchambua na kuchakata taka. Tunahitaji kuanza kufanya kazi hiyo vizuri zaidi katika wilaya yetu ya Rombo, ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuwafanya watu waweze kubadilisha mtazamo na mawazo yao juu ya usimamizi na matumizi ya taka baada ya kuzichambua na kuzichakata”. Alisema Hokororo
Wilaya ya Rombo ina mengi ya kujifunza kutoka katika Alvsbyn ambapo tunalenga kuboresha huduma za afya, hasa kwa vijana na jambo moja muhimu ni kuzuia mimba zisizotarajiwa mapema miongoni mwa vijana.Ndugu zetu wa Alvsbyn pia wanayo mengi ya kujifunza kutoka Rombo, kwa mfano, utalii wa asili na maendeleo ya uzalishaji wa chakula cha asili ili kuongeza kiwango cha kujitegemea miongoni mwa wananchi,alimalizia Hokororo
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved