Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara wasikwepe kulipa kodi zilizoruhusiwa na serikali alipokuwa anawahutubia wananchi wa Tarakea wilayani Rombo.
“Kwa kutazama tu eneo hili ni la biashara hivyo kwa wale wafanyabiashara tulipeni kodi,kwasababu kodi zenye kuudhi wananchi serikali imeziondosha na kuzipiga marufuku, lakini zile zilizoruhusiwa mzilipe ili lipatikane fungu zuri lifanye maendeleo pote Tanzania, Serikali hii inafanya maendeleo kwa fedha yetu wenyewe, msaada baadae”,alisema Samia
Mhe.Samia amefanya ziara wilayani Rombo mnamo Tarehe 9.11.2018 kwa lengo la kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo zinavyotekelezwa na serikali ya wilaya pamoja na Halmashauri ya wilaya na pia kusikiliza changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Katika ziara aliyoifanya wilayani Rombo alifanikiwa kutembelea ujenzi wa jengo la utawala, mradi wa maji Shimbi Mashariki pamoja na Msitu wa Rongai.
Mhe. Samia alitembelea ujenzi wa jengo la Utawala ,ambao bado haujakamilika kwasababu ya kukosekana kwa fedha, na kuahidi kuwa fedha za kumalizia ujenzi huo zitakuja ila zinaweza kuchelewa kwa sababu changamoto ni nyingi na mahitaji ni mengi lakini kipaumbele cha serikali ni kuboresha huduma zinazogusa wananchi moja kwa moja kama maji, elimu na afya.
Naye Waziri wa TAMISEMI Sulemani Jaffo alieambatana na Mhe.Samia katika ziara hiyo alisema kuwa serikali inawajali sana wananchi ambapo ndani ya mpango wa kuboresha vituo vya Afya nchini ndani ya miezi 18 vituo 350 vya afya vimekarabatiwa na kujengwa na vinatoa huduma ya upasuaji, na kwa idadi hiyo rekodi imevunjwa kwani toka uhuru mpaka mwaka 2015 vituo vya afya 115 tu Tanzania nzima ndio vilikuwa vinatoa huduma ya upasuaji.
Aliongeza kuwa serikali imeona pia changamoto nyingine ya kutumia hospitali Teule (DDH) katika wilaya ya Rombo na katika mpango wa serkali wa kujenga Hospitali za wilaya 167, wilaya ya Rombo ni mojawapo na tayari awamu ya kwanza ya fedha hizo shilingi 500,000,000 zimeshaingia katika akaunti ya Halmashauri.
Mhe. Samia akiwa katika mradi wa maji shimbi Mashariki alizungumza na wananchi wa vijiji vya Shimbi Mashariki na Munga ambao ni wanufaika wa mradi huo na kuwaahidi mradi utakamilika na wananchi kupata maji ifikapo mwezi wa tatu mwakani .
Aliongeza kuwa mradi ameuona na kimebaki kitu kidogo sana cha kuunganisha maji kutoka kwenye kisima kuingiza kwenye tanki na kuweka pampu kubwa itakayopeleka kwenye tanki kubwa ili yaende kwa wananchi, hivyo kwa pamoja na Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jaffo aliyeambatana nae katika ziara hiyo watawasiliana na Waziri wa Maji ili atafute fungu la kumalizia mradi huo.
“Tulipoingia madarakani tulitoa ahadi ya kuhakikisha tunapunguza au kuondosha kero ya maji nchini na kumsogezea mama huduma ya maji chini ya umbali wa mita 400 kwasababu tulitoa ahadi na mnajua serikali ya awamu hii inakwenda na ahadi zake na Mhe. Rais ni mtu wa kusema na kutenda hivyo na hili atalitenda na maji yatapatikana”.amesema Samia
Mhe.Samia pia alitembelea msitu wa Rongai na kukuta mapokezi makubwa ya wananchi ambao alizungumza nao na kuwaambia lengo kubwa la kutembelea msitu huo ni kuona jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Misitu Tanzania katika kutunza mazingira na kukuza Tanzania ya viwanda.
Aidha alisema kuwa ofisi yake inayojishughulisha na mazingira Tanzania imetoa agizo kwa kila wilaya(Halmashauri ya wilaya) kuhakikisha katika eneo lake la kiutawala inapanda miti 1,500,000 kwa mwaka. Miti hiyo inaweza kuwa miti mikubwa au miti midogo ya mimea kama Kahawa ambayo mbali na kurekebisha hali ya hewa pia inapendezesha na kujenga uchumi wa nchi.
“Nimeingia Rombo nimevuta hewa nyepesi na naihisi kabisa ni hewa safi na hii inasababishwa na kutunza miti,hivyo nawasihi pandeni miti kwa wingi kwa sababu tunapoelekea Tanzania ya viwanda moshi mwingi sana huzalishwa na viwanda na ili tuweze kuishi salama, moshi huu utanyonywa na miti tutakayoipanda”, amesema Mhe. Samia
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved