Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo amesisitiza wajibu wa viongozi, watumishi na wananchi katika uchaguzi, ili kuhakikisha unafanyika katika hali ya utengemano mkubwa,na kutimiza lengo la serikali la kuongeza usimamizi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa kuzingatia ubetuaji wa madaraka.
Akizungumza katika kikao maalum cha kutoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa Hokororo amewaambia wadau walioalikwa katika kikao hicho ambao ni viongozi wa taasisi na jumuiya mbalimbali, viongozi wa dini,vyama vya siasa,madiwani pamoja na watumishi wa serikali kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kanuni na miongozo iliyotolewa kuelekeza uchaguzi inatumiwa kwa umakini na uangalifu wa hali ya juu.
“Mwongozo wa elimu ya mpiga kura unatuhusu sisi sote kwasababu tuna dhamana na wajibu wa kuhakikisha elimu inayotolewa ni sahihi na inazingatia mambo muhimu ambayo mwananchi anatakiwa kuelezwa bila kutoka nje ya mstari”, amesema Hokororo
Sambamba na hilo ametoa angalizo kuwa, wananchi wapewe elimu na uhamasishaji wa kwenda kujiandikisha kupiga kura ifikapo tarehe 8 hadi 14 octoba ili watumie haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi,kwasababu baadhi yao wanaamini zoezi lililofanyika Julai 2019 la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo ni kwa ajili ya uchaguzi wa dola( uchaguzi mkuu) ndilo linalotumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Rombo, David Rubibira alitoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2019 kama kanuni inavyoelekeza kutoa maelekezo haya kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi , ukiwahusisha viongozi wa dini na wa vyama vya siasa.
Akitoa maelekezo hayo Rubibira ametaja tarehe rasmi ya uchaguzi ni 24 Novemba,2019 katika vituo vyote vilivyopo katika maeneo husika, tarehe ya uandikishaji wa wapiga kura ambayo ni tarehe 8 hadi 14 octoba, nafasi za uongozi zinazogombaniwa ( uenyekiti wa kijiji, ujumbe wa halmashauri ya kijiji na uenyekiti wa kitongoji) pamoja na sifa za mgombea na mpiga kura.
Pia alitolea maelekezo ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea uongozi, ukomo wa madaraka na uendeshaji wa mikutano ya kampeni za uchaguzi huku akisisitiza uchaguzi kuwa huru na haki ili kuhakikisha demokrasia inatendeka, na kukataza vitendo vya rushwa, maneno ya kashfa na lugha za matusi, ubaguzi wa aina yeyote na kutoa maneno yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Hata hivyo Mbunge wa Rombo Mhe. Joseph Selasini ambaye amehudhuria katika kikao hicho amehitaji ufafanuzi zaidi kuhusu uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea, na ametaka kujua ni ipi ngazi ya chini kabisa ya udhamini wa chama kwa mgombea .
Rubibira ametolea ufafanuzi zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea kwa kufuata kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji kanuni ya 17 kanuni ndogo ya(1) na ya (2) zinazoeleka mgombea atachukua fomu siku ishirini na sita kabla ya uchaguzi (29 Oktoba) na kurejesha ndani ya muda wa siku saba tangu siku ya kwanza ya uchukuaji wa fomu (29 Oktoba hadi 4 Novemba).
Aidha amefafanua kuhusu suala la udhamini wa vyama vya siasa kwa wagombea, kwa mujibu wa Mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ambao umezingatia kwamba, kila chama kina utaratibu wake wa kuteua au kutoa udhamini kwa wagombea wake.
l
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved