Picha kwa hisani ya mtandao
Mkuu wa wilaya ya Rombo Mhe.Agness Hokororo amekemea vitendo vya watumishi wa umma kuvutia au kuonesha dalili za kutaka kupewa rushwa pindi wanapotoa huduma kwa wananchi.
Akifungua semina ya siku moja ya mafunzo kwa watumishi wa umma dhidi ya rushwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo leo tarehe 30 Novemba, 2018, Hokororo amesema kuwa, mtumishi wa umma anapaswa kuwa kioo kwa kuhakikisha anakuwa msafi dhidi ya rushwa.
"Kama mtumishi wa umma ,uwe serikali kuu au serikali za mitaa, sisi ndio tunapaswa kuwa kioo kwasababu tunajua madhara ya rushwa kwamba inachelewesha maendeleo na inapoteza haki kwa ujumla wake,wananchi wanajua rushwa ni nini na dalili zake lakini katika maeneo mengi watumishi ndio wamegeuka mwiba badala ya kioo", amesema Hokororo
Ameongeza kuwa serikali imeamua kupambana na rushwa kwa vitendo na haitaacha mkubwa wala mdogo kinachotakiwa ni wananchi wote kupata huduma kwa kufuata taratibu kwasababu kupata huduma ni haki yao ya msingi.
Naye afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro Ndg Joseph Makuru ambaye ndiye mtoa mada ameanza kwa kuwaasa watumishi kuwa wanatakiwa kubadilika badala ya kupokea rushwa ni vema kushiriki kuwakamata wale wanaotaka kuwapa rushwa.
Makuru ameelezea vifungu mbalimbali vya sheria ya rushwa ya TAKUKURU ya mwaka 2007 ili kukuza ufahamu wa suala zima la rushwa kwa watumishi wa umma na kujua jinsi ya kuepukana nazo baadhi ya vifungu hivyo vinahusu kubadilisha matumizi ya fedha, rushwa katika ajira,matumizi mabaya ya mamlaka,mali zisizoelezeka upatikanaji wake na kughushi nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha.
Akitolea ufafanuzi kifungu namba 29 cha sheria ya kupambana na rushwa amesema kuwa ni kosa kisheria kubadili matumizi ya fedha za serikali na pale inapohitajika kufanya hivyo ni budi kupata kibali kutoka kwa wahusika walioleta fedha hizo ikiambatana na sababu ya msingi ya kutaka kubadili matumizi.
Kifungu namba 22, kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri; nyaraka,stakabadhi,Ankara,karatasi za kumbukumbu zinazohusu shughuli za mwajiri zikiwa na maelezo ya uongo kwa kuandaa vikao hewa,bajeti na vifungu ambavyo havipo orodha ya majina ya washiriki na sahihi za kughushi , huu ni uhalifu mkubwa uliofanyiwa mipango ndio ukatendeka.
Hata hivyo ametolea msisitizo kuwa kuna mazingira mengi ya rushwa katika taratibu za manunuzi ya serikali, na hata kutoka nje ya kituo cha kazi bila ruhusa ya mwajiri pia ni kuhujumu uchumi na ni kosa kisheria kwa sababu serikali inalipa mshahara ikiamini mtumishi anafanya kazi kwa masaa ambayo anatakiwa kuwa kazini.
Amemalizia kwa kutoa onyo kali kwa kutumia kifungu namba 52 cha sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007 kuwa ni kosa kisheria kumtishia mtu anayetoa taarifa za rushwa TAKUKURU
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved