Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Raisi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza ahadi zake za kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali za wilaya kwa wilaya ambazo hazikuwa na hospitali hizo ikiwa ni pamoja na wilaya ya Rombo.
Serikali iliahidi kutoa kiasi cha fedha za kitanzania shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na tayari awamu ya kwanza ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 500 zimeshapokelewa na ujenzi utaanza mara baada ya wizara husika kujiridhisha na eneo litakalotumika kujenga hospitali hiyo pamoja na ramani.
Taarifa ya ujio wa fedha hizo ilijadiliwa katika kikao cha kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango cha Tarehe 23.10.2018 ambapo Mhe.Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo amewapongeza wataalamu wa Halmashauri kupitia Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kufanya utafiti na kupata eneo litakalofaa kwa ujenzi wa hospitali katika kata ya kirongo samanga, kijiji cha Kiwanda kitongoji cha Mteri.
“Eneo hilo ni la umma na lilikua likitumika kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja na serikali ya kijiji kukodisha ardhi kwa wananchi kwa ajili ya kilimo cha mazao ya muda mfupi, na hilo lilikuwa likitendeka ndani ya sheria iliyoanzisha mamlaka ya serikali za mitaa ya mwaka 1984, ambayo inatoa mamlaka ya ardhi ya kijiji kusimamiwa na serikali ya kijiji”, alisema Hokororo
Aliongeza kuwa mpango utakaofuata ni kufuata taratibu za kisheria na kuhawilisha matumizi ya ardhi hiyo, ili kuwezesha uandaaji wa mchoro wa viwanja katika eneo hilo zoezi litakalosimamiwa na Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira hatua kwa hatua na hatimaye umiliki wake upate Hati miliki ya muda mrefu .
Naye Mhe.Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ,Evarist Silayo aliwasihi madiwani wa halmashauri kuungana na ofisi ya Mkuu wa wilaya pamoja na watendaji wa halmashauri na kuwa kitu kimoja ili waweze kuzungumza na wananchi hasa katika kijiji cha kiwanda na wakulima wote waliokuwa wanakodi maeneo ya kulima katika eneo hilo kwa lengo la kuwapa taarifa ya ujenzi wa hospitali katika eneo.
Awali mpango wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo ilikuwa ni kukipandisha hadhi kituo cha afya Karume ili kuwa hospitali ya wilaya lakini serikali ilikataa ombi hilo, na badala yake ndani ya mpango wa serikali wa kuimarisha sekta ya afya hususani afya ya Mama na Mtoto wilaya ya Rombo ilipokea kiasi cha shilingi milioni 500 zilizotumika kujenga na kukarabati baadhi ya majengo katika kituo cha afya Karume na kuifanya iwe na hadhi ya hospitali.
Hivyo, ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Rombo utazidi kuimarisha huduma za Afya kwa wananchi wa Rombo ambao mpaka sasa wanatumia Hospitali ya Huruma inayomilikiwa na kanisa katoliki kama hospitali teule ya wilaya ( DDH-District Designated Hospital),.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
simu: 027-2757101
Mobile: 027-2757101
staff mail: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved