Wananchi wa vijiji vya Katangara na Mrere wameridhia kuchangia deni la wazabuni kiasi cha shilingi milioni 23,744,000.00 ambalo limetokana na kukopa vifaa vya ujenzi wa maabara ya kisasa ya baiolojia na fizikia katika shule ya sekondari Mashati.
Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ambao ni Afisa Mipango, Mkaguzi wa ndani, Mwanasheria pamoja na Afisa Elimu sekondari kufanya mkutano na wananchi wa vijiji hivyo wakishirikiana na bodi ya shule, kamati ya ujenzi ya shule pamoja na uongozi wa vijiji na kujadili namna ya kulipa deni la mzabuni ambaye amepeleka kesi mahakamani ili kulipwa deni lake.
Baada ya wananchi kusomewa taarifa kamili ya mradi na madeni ambayo mradi huo unadaiwa, wananchi waliridhia kulipa deni hilo kidogo kidogo kwa awamu kwa kila kaya kuchangia shilingi elfu thelathini(30,000) kwa kuanza na zile kaya ambazo hazijachanga kabisa kwa uwiano wa shilingi 15,780,000 kijiji cha Mrere na shilingi 8,000,000.00 kijiji cha katangara ili kulipa deni lote ambalo mradi huo unadaiwa.
Aidha mradi wa maabara ya Mashati sekondari ni mradi ambao ulikataliwa kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka jana kutokana na mzabuni kutokulipwa deni lake ,na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo kuhakikisha anamlipa mzabuni aliyetoa vifaa vya ujenzi ndugu Sabas Shirima kiasi cha shilingi milioni 22,744,000.00 ambapo kiasi cha shilingi milioni kumi (10,000,000) kililipwa na halmashauri na kiasi kilichobaki kilitakiwa kulipwa kutokana na michango ya wananchi.
Hata hivyo baada ya Ofisi ya Mkurugenzi kulipa kiasi alichotakiwa kulipa bado upande wa wananchi hakuna malipo yeyote yaliyofanyika kitu kilichopelekea mdai kurudi mahakamani ili kukazia hukumu ili amaliziwe deni lake lote, hatua ambayo ilibidi Mkurugenzi Mtendaji Bi Magreth L John na timu ya wataalamu kujipanga upya kwenda kuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo.
Katika mkutano huo wananchi waliridhia kulipa deni hilo lililobaki kiasi cha shilingi milioni 12,744,000.00 la ndugu Sabas Shirima lakini pia walikubaliana walipe madeni yote ya mradi huo wanaodaiwa na wazabuni pamoja na mafundi ili kuepuka usumbufu, ambapo jumla ya deni ambalo mradi huo unadaiwa ni shilingi 23,744,000.00
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved