Halmashauri ya wilaya ya Rombo imetoa mkopo wa shilingi milioni 61.5 kwa jumla ya vikundi 20, vya wanawake (12), Vijana ( 7) na wenye ulemavu ( 1), kupitia 10%(asilimia kumi) ya mapato ya ndani ,ambayo kwa mujibu wa sheria ni lazima iende kwenye makundi hayo ili kuyainua kiuchumi.
Afisa Maendeleo ya Jamii (W) Patricia Kinyange ameeleza kuwa vikundi vilivyokuwa vimeomba mkopo vilikuwa 55 vilivyokuwa na thamani ya milioni 275 lakini kutokana na mapato madogo ya Halmashauri kamati ya wilaya ilikaa na kuchuja angalau kila Kata ipate kikundi kimoja na baada ya mchujo vilipatikana vikundi 20 ambavyo ndivyo vinavyopokea mkopo huo.
Ameongeza kuwa mikopo hii inayotolewa sasa ni ya kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2019/2020, na hivi karibuni halmashauri inategemea kumalizia kutoa mikopo kwa robo ya pili.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe. Agness Hokororo amevitaka vikundi vilivyopata mkopo kufanya biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu huku wakijifunza kutunza akiba zao zitakazowasaidia kufanya uzalishaji mkubwa zaidi, ili nia njema ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi ionekane .
Sambamba na hilo amewaasa wanavikundi kujiepusha na biashara za magendo, na kuweka wazi iwapo wakijihusisha, serikali itawakamata na fedha yote ya kikundi itapotea na kuwasababishia hasara na kushindwa kufanya marejesho kitu kitakachopelekea Halmashauri kuwashitaki mahakamani.
“Natamani vikundi hivi viendelee kiuchumi na baadae hata kuungana na kuwa na mtaji mkubwa zaidi ili kuanzisha viwanda vitakavyokuwa vinatengeneza bidhaa zilizoongezwa thamani na bidhaa za uzalishaji ambazo zitakuwa zinatoka Rombo,” amezungumza Godwin Chacha ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo.
Kabla ya kupewa mikopo hiyo vikundi hivyo vilipata mafunzo ya siku mbili juu ya uandaaji wa vitabu vya fedha vinavyotunza kumbukumbu, Elimu ya ujasiriamali,usimamizi wa akaunti , hatua za kuchukua kabla ya kuchukua mkopo, namna ya kufanya marejesho na jinsi ya kujisajili PPRA.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved