Mkuu wa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Raymond Mwangwala amewataka wazazi wote wenye watoto wa umri wa kuanza shule, kuhakikisha wanawaandikisha na kwamba kwa wale ambao watakiuka hilo, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kushtakiwa.
Mwangwala ametoa rai hiyo leo jumatatu, januari 15,2024 baada ya kufanya ukaguzi katika baadhi ya shule ikiwemo shule ya Msingi ubaa ili kuangalia hali ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza
"Wanafunzi wameweza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha darasa la kwanza na awali, zipo shule ambazo zimevuka malengo ikiwemo shule ya Msingi Ubaa ambayo maoteo kwa darasa la awali ilikuwa ni wanafunzi 22 lakini mpaka sasa wameandikishwa 60 lakini darasa la kwanza wanafunzi waliopaswa kuandikishwa ni 30 lakini tayari wameandikishwa 40".
Aidha mkuu huyo amesema tayari wameanza msako wa nyumba kwa nyumba na hata kwenye magulio na Masoko ili kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda ili kutimiza haki zao za kimsingi za kupata elimu.
"Kwa sasa viongozi kuanzia ngazi za vitongoji, Kata, Tarafa na Hata Wilaya, wameanza kuzunguka kuanzia kwenye vitongoji nyumba kwa nyumba wakiongozwa na mimi kiongozi wao kuhakikisha watoto wote wanaopaswa kupelekwa shule, wanapelekwa"
"Tutachukua hatua kali za kisheria ikiwemo kuwashitaki wazazi ambao hawatawapeleka watoto shule ili hali umri wa kwenda shule umefika. Mtoto kupata elimu ni haki ya msingi ya binadamu hivyo tutachukua hatua kwa yeyote ambaye atakiuka haki hii ya msingi".
Mkuu huyo ametoa pia wito kwa jamii, kuwaripoti watoto wote wenye umri wa kwenda shule ambao wanazurura mitaani au wameachwa nyumbani ili hatua zichukuliwe kwa wazazi.
Ametumia pia nafasi hiyo kuwataka walimu kutimiza wajibu wao wa kuwafundisha wanafunzi ili kuwawezesha kupata elimu bora kama ilivyokusudiwa.
Mpaka kufikia Januari 11,2024 katika Wilaya hiyo tayari wameandikisha wanafunzi 4,639 wa awali na wanafunzi 4,454 wa darasa la kwa kwanza ikiwa ni asilimia 90 ya malengo yaliyowekwa.
KUONA VIDEO BOFYA LINK HAPA CHINI.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved