Kiasi cha shilingi Milioni 138.6 zawanufaisha Vijana 401 wilayani Rombo kupitia mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na walemavu ambao unatokana na asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani ambapo 4% ni ya wanawake, 4% ya Vijana na 2% ya walemavu.
Hayo ameyasema Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo Ndugu Magreth L John alipokuwa akitoa taarifa kwa wajumbe kutoka ofisi ya Waziri Mkuu ambao ni Maafisa Maendeleo ya Vijana walipozuru wilayani Rombo leo tarehe 17.6.2019 ili kukagua asilimia nne (4%) ya mapato ya ndani ambayo Halmashauri inatakiwa kukopesha vikundi vya vijana bila riba.
Ndugu Magreth ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/17 kiasi cha shilingi 10,600,000.00 zilitolewa kwa vikundi saba vyenye jumla ya watu 88, mwaka wa fedha2017/18 kiasi cha shilingi 46,500,000.00 kilitolewa kwa vikundi 22 vyenye jumla ya watu 217,na mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha shilingi 49,500,000.00 kimeshatolewa kwa vikundi 12 vyenye watu 96.
Ameongeza kuna vikundi vingi vya vijana vinaendelea kuwezeshwa kwa awamu kulingana na hali ya makusanyo na uwepo wa fedha, sambamba na hilo Halmashauri ya wilaya kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kutoa elimu ya mikopo na ujasiriamali kwa kuwazungukia vijana vijijini.
Akizungumzia mafanikio yaliyoonekana ni pamoja na kufanikiwa kulipa deni la mkopo wa Wizara kiasi cha shilingi milioni 16, na kupokea fedha ya marejesho kiasi cha shilingi milioni 32 ambazo nazo zimekopeshwa vikundi vya vijana
Aidha changamoto kubwa ni vijana kujiunga kwenye vikundi ili wapate mikopo lakini wakishapata wanasambaratika na kugawana fedha hivyo ili Halmashauri ipate marejesho imebidi Halmashauri ishughulike na wadhamini wao kwa sababu kila kikundi inabidi kiwe na wadhamini hivyo wao ndio wanaobanwa ili tupate marejesho.
Naye Ndugu Godfrey Nyaisa ambaye ni Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana ,Ajira na walemavu aalisifia jitihada zinazofanywa na Halmashauri kwa kuhakikisha Vijana wanakopeshwa kupitia 4% na inaonekana kweli vijana wanachapa kazi kulingana na kasi yao ya marejesho.
Nchi inatengenezwa na vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa na ndio wanategemewa waweze kusaidia azma ya taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025,hivyo ni budi halmashauri kuendelea kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi na kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
"Lengo la serikali ni kutaka vijana wawezeshwe ili waweze kujiajiri , na tumefurahishwa kusikia vijana wamemaliza deni lao la mkopo wa Wizara kwasababu katika halmashauri nyingi nchini kumekuwa na changamoto sana kwenye urejeshaji wa mikopo kuna maeneo mengine madeni ni makubwa na waliokopa hawajulikani walipo na wengine hawatambuliki", ameyasema haya Ndugu Amina Sanga Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana ,Ajira na walemavu.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved