Hofu iliyokuwa miongoni mwa waheshimiwa madiwani juu ya nyama zisizokaguliwa na wataalamu wa mifugo kuuzwa na kuliwa na wananchi imeondolewa baada ya Daktari wa Mifugo Dr Emil Mkemwa kuwahakikishia kuwa nyama zote zinazouzwa kwenye mabucha rasmi zimekaguliwa na ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Waheshimiwa madiwani waliibua hoja hiyo katika kikao cha kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira, ambapo walizungumza kwa nyakati tofauti tofauti na kukihakikishia kikao kuwa kuna baadhi ya wafugaji ambapo hujifanya wao ni wataalamu wa mifugo na kuchinja mifugo na kuuzia wananchi bila kukaguliwa na wataalamu kitu ambacho kinahatarisha maisha ya wananchi wa Rombo.
Akijibu hoja hiyo Dr Mkemwa amesema kuwa japokuwa kuna changamoto ya Idara ya Mifugo kuwa na wataalamu wa Mifugo 15 tu, lakini kwa uchache wao hujipanga na kuhakikisha nyama zote zinazochinjwa na kuuzwa kwenye mabucha rasmi zinakaguliwa na ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Hata hivyo ameomba ushirikiano baina ya wataalamu wa mifugo na waheshimiwa madiwani kupeana taarifa iwapo kuna wafugaji na wafanyabiashara wasio waaminifu katika maeneo yao, ambao wanawakwepa wataalamu wa mifugo na kuchinja mifugo inayoumwa bila kujua imeumwa nini au kuuza nyama ya mizoga ili hatua stahiki zichukuliwe.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Athuman Kimaryo diwani wa kata ya Mrao Keryo amesema kuwa kiuhalisia bado wananchi wengi wanakula nyama ambayo haijakaguliwa kwasababu kuna wananchi wanachinja saa 9 usiku na ikifika saa 11 alfajiri nyama imeshauzwa imemalizika na pindi mtaalamu wa mifugo akifika hakuti kitu, hivyo tatizo kubwa analoliona hapo ni uhaba wa wataalamu na baadhi yao si waaminifu.
Naye diwani wa Kata ya Tarakea Motamburu Mhe. Beda Moshi amesema kuwa sio rahisi kwa wataalamu kuwapitia wananchi wote hata kama wakiwepo wanne katika kata moja kwasababu kila mtu anachinjia nyumbani tena wanyama wanaochinjwa ni tofauti tofauti hivyo bado usalama wa nyama zinazoliwa na wananchi ni mdogo ila anaona ingekuwa vyema kama kungekuwa na centre maalumu ya kuchinjia ingekuwa rahisi zaidi kufanyiwa ukaguzi.
Rombo District Council,Mkuu Bomani Street
Sanduku la Posta: P.o Box 52,Mkuu,Rombo
Simu: 027-2757101
Simu ya Mkononi: 027-2757101
Barua Pepe: ded@rombodc.go.tz
Copyright@2019Rombodc.all rights reserved